
Hapa nipo na washikaji zangu wakubwa

ANAKULIZA KILA MARA LAKINI UNASHINDA KUMUACHA?
....Makala hii itakusaidia sana!
Namshukuru Mungu kwa mara nyingine tena kwa kunijaalia fursa hii adhimu ya kuzungumza nanyi wapenzi wasomaji wa safu hii ya uwanja wa mapenzi. Jamani mambo vipi? Wiki ya mashamsham ya wapendanao ilikwendaje? Natumaini ilikuwa bab kubwa! Au siyo!
Haya karibuni tena kwenye ‘mambo yetu yale’ ya malavudave, si unajua bila mapenzi hakuna maisha! Huo ndio ukweli, huwezi kuishi kama jiwe au mti. Raha ya maisha ni kuwa na mwenzi, mpenzi wa kumpenda na kukupenda ki ukweli na sio kujaribu au kuzuga.
Kwa wale walio katika mapenzi matamu na ya kweli watakubaliana na mimi kuwa mapenzi yenye amani na masikilizano ni kama ‘ka paradiso’ kadogo ndani ya ulimwengu huu mkubwa uliojaa vituko! Wakati mwingine unaweza hata kujikuta umeshiba bila kula, eti kwa sababu tu umemuona mpenzio au kuwa nae karibu tu yaani yeye kwako ndo’ mambo yote, yeye ndio kila kitu! Raha ilioje!
Wakati wengine wakiishi kwa raha katika maisha yao ya kimapenzi, wapo wengine wanaoishi na wapenzi wao huku mioyo yao ikiwa imesinyaa! Kila siku ni karaha na vituko vya makusudi kutoka kwa wapenzi wao japo wanawapenda sana na kuonesha mapenzi yao yote. Kila siku ni maumivu na simanzi ya moyo isiyojulikana mwisho wake.
Lakini pamoja na karaha, vituko na dharau zinazofanywa na wale tuwapendao bado kuna wale wenzangu na mimi utakaowasikia wakisema “Ah! Nitavumilia tu, labda atabadilika na nafikiri sitoweza kumuacha kwa kuwa nampenda sana!”
Jamani, huenda nikawa na msimamo tofauti kidogo, lakini mimi naamini kuwa mapenzi ya kweli ni pamoja na kumsikiliza mwenzio na kuheshimu hisia zake, hasa katika mambo yanayofaa. Tofauti na hapo, tabia ya kutokuwa msikivu, kutojali na kutokuwa mwepesi kubadilika ni dalili tosha ya kutokuwepo kwa upendo wa kweli na wa dhati. Mapenzi nijuavyo mimi ni kupenda, kupendwa, kusikizana na kuheshimiana na si vinginevyo!
Hata hivyo naomba nichukue nafasi hii kuwapa pole wale wote wanokwazwa na wapenzi wao kwa namna moja au nyingine kwa sababu mbalimbali kama vile usaliti katika mapenzi, ulevi, ujeuri, kutojali, vipigo na ubabe na mengineyo mengi.
Na pia nafahamu kuwa wakati mwingine unajikuta katika wakati mgumu wa kuamua hatma ya uhusiano wako na mpenzio kwa kuwa unahisi unampenda sana na kwamba hauko tayari kumkosa maishani. Labda tubadilishane mawazo, kama wewe ni mmoja wapo kati ya wanaokabiliwa na hali hii. Hebu jaribu kupitia dondoo zifuatazo
Mueleze jinsi unavyokwazika
Ni vizuri kabla hujaanza kulalamika kwa watu wa pembeni, hakikisha unamwambia ukweli mwenzi wako juu ya tabia yake na kumueleza ni jinsi gani unaumizwa mno na tabia hiyo.Lakini hakikisha unaongea nae katika hali ya upendo na sio kuporomosha lawama na kubwatuka hovyo, la sivyo atakugeuzia kibao na mtakosana zaidi.
Ana dalili ya kubadilika?
Kwa mpenzi anayeonesha angalau kubadilika ni heri kwako, lakini kwa wale “sugu” ambao wanaendeleza tabia zao hata mwaka mzima na kuwa hodari sana wa “samahani honey, si unajua binadamu hukosea na kujisahau, nisamehe mpenzi.” Hivi hii ni samahani gani wakati unarudia makosa yale yale kila kukicha, mpenzi wako akueleweje kama sio kumdharau. Ukiwa na mtu wa namna hii, mtazame vizuri kisha uamue!
Tabia yake inavumilika?
Jamani kuna mambo mengine madogo madogo yanaweza kuvumilika kwa kuwa huenda “sio ishu sana.” Lakini kuna tabia nyingine huna haja ya kuzifumbia macho na kujiongopea kuzivumilia. Kwa mfano tabia ya vipigo kila siku, utavumilia mpaka utakapotolewa macho au unyofolewe na roho yenyewe kabisa au? Mpenzi Malaya, utamvumilia mpaka pale atakapokuletea Ukimwi uhangaike nao? Sidhani kama ni busara kuvumilia haya, usikubali kabisa kupelekwa pelekwa na hiyo hisia yako ya “lakini nampensa sana!” Hebu jiangalie vizuri.
Omba ushauri
Wakati mwingine ni vyema sana ukawaomba watu ushauri juu ya nini ufanye unapokabiliwa na msongo wa mawazo unaotokana na kero za mpenzi wako. Kwa wanandoa wanaweza kuwahusisha wazee na wakati mwingine hata vyombo vya sheria. Usikubali kunyamaza na “kumezea” matatizo uliyo nayo, utakufa kihoro buree! Waombe ushauri wale unaowaamini huenda wakakuonesha njia.
Jifunze kwa wengine
Jiulize, hivi ni wangapi unaowafahamu na wengine kusikia habari zao, ambao waliwahi kupenda kama wewe lakini kutokana na manyanyaso na kutosikilizana wameachana na wapenzi wao, na sasa wanaishi maisha mengine matam na wapenzi wao wapya, kwanini usiwe wewe?
Ondokana na “siwezi kuishi bila yeye”
Pamoja na yote, ukweli unabaki palepale kwamba kuamua, “kummwaga” mtu unayempenda si kazi ndogo, lakini inafikia mahali inakuwa haina jinsi inakubidi. Uwe jasiri ili uondokane na maisha ya “roho juu juu” kila siku! Potelea mbali ili mradi upate uhuru wa nafsi.
Amini wa kwako aja!
Amini kuwa huenda Mungu hakukupangia ufurahi maisha na huyo uliye naye sasa kwa kuwa yule wako “original” bado yu njiani na kusahau machungu yaliyopita Inshaallah!
Assalam Alaikum! Ni furaha yangu kwa mara nyingine tena kukutana nanyi wapendwa wasomaji wa safu yetu hii ya uwanja wa mapenzi. Tumshukuru Muumba wetu kwa kutujaalia uhai na afya njema, lakini zaidi ya hapo tumshukuru pia kwa kutuumbia kitu mapenzi au sio?
Siku zote hatutaacha kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapenzi ndio maisha yetu. Tunafanya kazi usiku na mchana, tunahangaika huku na huko, lakini mwisho wa siku tunafikiria jinsi gani tutapata kuboresha na kufurahia maisha na wapenzi wetu. Tunafikiria pia ni jinsi gani tunaweza tukapata utulivu na amani katika maisha ya kimapenzi na wapenzi wetu, waume zetu au wake zetu katika siku zote za maisha yetu.
Wiki hii nimeona ni vyema tukabadilishana uzoefu juu ya suala zima la wivu katika mapenzi. Mtakubaliana nami kuwa suala la kuwa na wivu kwa mpenzi wako ni jambo lisilokwepeka hasa kwa sababu kubwa ya kuaminika kwake kwamba kuwa na wivu ni moja ya kigezo cha kuonesha ni jinsi gani unampenda mpenzio na kwamba hauko tayari kwa namna yoyote ile kushea na mwingine ndio maana wanawake wengi hawataki kusikia suala la ukewenza kabisaa! Hata kama jambo hilo limepewa baraka zote na dini au tamaduni zao.
Lakini kubwa katika wivu ni ile kutokuwa tayari kuona tunasalitiwa na wapenzi na hasa kwa wale tunaowapenda ukweli toka moyoni mwetu na zaidi ukute ndo tumeshawagharamikia kiasi cha kutosha na kujitoa kwao kwa kila kitu!
Umeshawahi kusikia kauli kama “Jamani mke (au mume) anauma! Au kauli kama mke wa mtu sumu” na hugeuka sumu kweli hasa pale “unapobambwa” na mali za wenyewe, kufanyiwa “kitu mbaya” inakuwa sio jambo la ajabu sana.
Niwaambie kitu wapenzi wasomaji! Mapenzi bwana ni “full uchoyo, ni full kujipendelea! Mpenzi wanaume kwa mfano, anaweza kufikiria kwamba ni yeye tu ndiye anayestahili na anayeweza kumfanya mpenzi wake acheke na kufurahi.
Na kwamba akitokea mwanaume mwingine akapata nafasi ya kumfurahisha mpenzi huyo hata katika stori za kawaida tu, unaweza ukasikia akisema, “Hivi wewe mna nini na huyo jamaa, mbona unamchekea chekea hivyo, au…!” Hiyo ndiyo choyo ya penzi, na kikubwa kinachofanyika hapo ni ile tu kujaribu kulinda maslahi binafsi.
Pamoja na ukweli kwamba tabia ya wivu inapozidi hugeuka kuwa kero, lakini kabla hatujafika huko hebu tuangalie nafasi ya wivu katika mapenzi yetu. Yaani swali ni kwamba, je! Wivu katika mapenzi unaleta maana?
Nionavyo mimi wivu ukitumika vizuri unaleta maana na una nafasi muhimu sana katika mapenzi kwa sababu zifuatazo:
Huonesha kujali
Sote tunaamini pasipo na wivu hata chembe, hapana mapenzi ya kweli. Kumuonesha wivu mpenzi wako ni kumjulisha ni kiasi gani unamjali na kumpenda na kwamba yeye ni mtu maalum sana kwako.
Jamani, mahali penye mapenzi yasiyo na wivu hata kidogo, panatia shaka! Na mara nyingi majibu yake ni kutokuwa “sirias” katika uhusiano huo au huenda kuna kupitisha muda tu na kwamba labda hakuna “future” na mpenzi huyo au ni dalili ya kuchuja kwa penzi.
Kuthamini uhusiano
“Sio kama sikuamini dear, bali wivu wangu kwako ni katika kuuthamini uhusiano wetu, mimi na wewe ni umoja wenye thamani kubwa, tusiruhusu kuuchezea nje yetu! Huu ni mfano wa ujumbe unaoonesha maana na nafasi ya wivu katika mahusiano ya kimapenzi.
Kukumbushana
Kauli au matendo yanayoashiria kumuonesha wivu mpenzio yanasaidia kwa kiasi kikubwa kumfanya mwenzi wako “asijisahau” katika jukumu la kulienzi penzi lenu hata akiwa mbali ya upeo wa macho yako.
Kujijengea heshima
Kwa namna moja au nyingine, wivu pia huweza kukujengea heshima. Kwa mfano mume mwenye wivu na mkewe hujijengea heshima ya kwamba kweli anamjali na kumpenda mkewe lakini pia anaweka mazingira ya kutosumbuliwa kwa mke wake huyo kumjengea heshima yake kama mke wa mtu.
Husaidia kubadilisha tabia
Ukiwa na wivu, unaotokana na mavazi “tatanishi” anayopendelea kuvaa mpenzi wako kwa mfano, huenda ikasaidia kubadili tabia yake.
“Ni kweli umependeza na umetoka “chicha” ile mbaya mpenzi, lakini mh! Naogopa wanaume wakware watakusumbua honey, unaonaje ukavaa simpo tu?” Kama anakupenda huenda akabadilika kidogo na hivyo “vivazi vyake”.